Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Spika wa bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko ameunga mkono hatua ya wawakilishi wadi kutaka kusimamia pesa za ustawishaji wa maeneo wadi.

Akihutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne, Nyamoko alisema kuwa wawakilishi wadi wana haki ya kusimamia pesa za ustawishaji wa maeneo wadi.

Nyamoko alisema kuwa ana imani kuwa pesa hizo zitatumika kwa manufaa ya wananchi.

"Kwa kweli sioni sababu ya kutoruhusu wawakilishi wadi kusimamia pesa za ustawishaji wa maeneo wadi kwa maana wao ndio wamekuwa wakizinikisha afisi ya mthibiti wa makadirio ya bajeti kuwaruhusu kusimamia pesa hizo. Nina hakika kwamba pesa hizo zitatumika vizuri kwa manufaa ya wananchi ikizingatiwa wawakilishi wadi ndio waliopo karibu na wananchi,” alisema Nyamoko.

Nyamoko vilevile alisema kuwa hali ya wawakilishi wadi kuwepo karibu na wananchi kutawawezesha kuwafanyia wananchi kazi bila ya ubaguzi, huku akiwahimiza wawakilishi wadi kuhakikisha pesa hizo zinawanufaisha wananchi.

"Wawakilishi wadi ndio walio karibu na wananchi na kwa maana hii itakuwa rahisi kutengea miradi muhumi pesa bila ya ubaguzi. Sasa lililo baki ni kwa wawakilishi wadi kuhakikisha kuwa pesa hizo zinawanufaisha wananchi," alisema Nyamoko.

Haya yanajiri baada ya bunge la kaunti hiyo kupitisha mswada uliowasilishwa na mwakilishi wa wadi ya Gesima, uliomtaka mthibiti wa bajeti za serikali Agnes Odhiambo kutenga pesa za ustawishaji maeneo wadi mswada ambao Odhiambo aliutia sahihi.