Share news tips with us here at Hivisasa

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyamira amewahiza vijana wa kaunti hiyo kuasi tabia ya kukumbatia siasa za kiukoo, kwa kuwa zimepitwa na wakati.

Akihutubia wakaazi wa Nyamusi siku ya Jumapili, Joash Nyamoko alisema kwamba siasa za kiukoo zinaathiri pakubwa maendeleo katika Kaunti ya Nyamira, na kuzua uhasama miongoni mwa koo mbalimbali.

“Nilifikiri kwamba tangu tupate rasimu ya katiba mpya iliyozileta serikali za ugatuzi, mambo yangelibadilika. Nimekuwa nikishuhudia baadhi ya wanasiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa wakiuza sera zao kwa wananchi kwa misingi ya kiukoo. Kama vijana mnastahili kusuta vikali dhana hii potovu," alisema Nyamoko.

Nyamoko aidha aliwahimiza vijana kuwachagua viongozi wenye maono bila ya kuzingatia ukoo wao, akihoji kuwa vijana wana usemi mkubwa wakuamua mstakabali wa taifa hili kisiasa, ikizingatiwa kwamba idadi yao ni kubwa.

“Ni ombi langu kwenu kuhakikisha kwamba mnawachagua viongozi wenye maono mazuri. Sio lazima muwachague wale viongozi wa zamani kwa kuwa mnaweza mchagua mmoja wenu," alisema Nyamoko.