Spika wa bunge la seneti Bw Ekwe Ethuro amewataka Wakenya wa matabaka yote kukumbatia mpango wa serikali wa kutaka Wakenya wote kuwa na bima ya afya.
Akihutubu wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la hospitali ya Mediheal mjini Eldoret Bw Ethuro alisema Wakenya watachukua bima inayokubalika kote ulimwenguni itasaidia kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa gharama ya matibabu.
Bw Ethuro alisema kuna haja ya Wakenya kuhamasishwa kwa kina kuhusu umuhimu wa bima ya afya.
Kinara huyo aliwataka Wakenya kuchangia kwa bima hiyo ili wawe wakinufaika nayo wakati wanapohitaji huduma za matibabu haswa matibabu spesheli.
"Tamanio la serikali kutaka kila Mkenya awe na bima ya afya ni mpango mzuri ambao unalenga kuona kwamba Wakenya wote wanamudu gharama ya matibabu spesheli,kulipa bima ya shilingi 100 au 200 kwa mwezi si nyingi ikilinganishwa na faida zake kwa mhusika,tujisatiti tuchukue bima hii kila mtu" alisema Ethuro
Ethuro alisema bima hiyo itawapunguzia Wakenya mzigo wa kufanya harambee za kugharamia matibabu.
Msimamo wa Ethuro uliungwa mkono na seneta Beatrice Elachi ambaye alisema kila mwezi Wakenya huchanga pesa za kuwasaidia wenzao kutafuta matibabu spesheli iwapo watachukua bima hiyo harambee za aina hiyo zitaepukwa.
Elachi ambaye ni kiranja wa serikali katika bunge la seneti alisema kuna haja ya kuondoa siasa katika swala nzima la la bima ya afya ili walengwa waweze kunufaika.