Spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko amewahimiza wawakilishi wadi wa bunge la kaunti ya Nyamira kufika mapema bungeni kwa minajili ya kuhudhuria vikao.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumanne, Nyamoko alisema kuwa yafaa wawakilishi wadi wafike mapema bungeni ili kujadili miswada muhimu kwa wakati.
"Nawaomba wawakilishi maeneo wadi kufika mapema bungeni wakati wa vikao ili kutuwezesha kujadili miswada muhimu hasa ya kustawisha kaunti hii kwa wakati," alisema Nyamoko.
Nyamoko aidha alisema kuwa huenda akalazimika kuwachukulia hatua za kinidhamu wawakilishi wadi walio na mazoea ya kufika bungeni kama wamechelewa na hata pia kukosa kufika bungeni bila ya spika kuwa na ufahamu.
"Naona wakati umefika kwangu kulazimika kuwachukulia hatua kali za kinidhamu baadhi ya wawakilishi wadi walio na mazoea ya kufika bungeni wakiwa wamechelewa, hasa wale walio na mazoea ya kukosa kuhudhuria vikao vya bunge wacha wajue kuwa wameonywa," aliongezea Nyamoko.