Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume mmoja wa umri wa makamo anaendelea kuzuiliwa na maafisa wa polisi mjini Nyamira baada yake kupatikana akiwatapeli wahudumu wa mikahawa kwa kujifanya kuwa afisa wa afya ya umma.

Akithibitisha kisa hicho afisa mkuu wa afya ya umma wilayani Nyamira kusini David Oyaro alisema mshukiwa alipatikana na lesenia bandia za biashara alizokuwa akizitumia kuwatapeli wakaazi wa Kebirigo.

"Ni kwa ushirikiano wa wananchi waliomshuku mwanamume huyo uliofanikisha maafisa wa polisi kumtia mbaroni kule Kebirigo alikokuwa akitumia leseni bandia za biashara ili kuwatapeli wananchi," alisema Oyaro.

Oyaro aliwaomba wananchi kuwa waangalifu kuwatambua matapeli wa aina hiyo ili kuwaripoti kwa maafisa wa polisi.

"Ni ombi langu kwa wananchi kuendelea kuwa waangalifu dhidi ya watu walio na mazoea kama haya na sharti wawe tayari kuripoti visa kama hivi kwa maafisa wa polisi ili hatua zichukuliwe," aliongezea Oyaro.

Kwa sasa mshukiwa huyo anaendelea kuzuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Nyamira akingoja kufikishwa mahakamani.