Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya lalama kuzidi kutoka kwa wakazi wa Kibuyuni, Wadi ya Bofu, mwakilishi wadi wa eneo hilo ameahidi kuwa atafanya kila juhudi kuondoa jaa la taka ambalo limekuwa kero kwa wakazi hao.

Alisema kuwa atashinikiza serikali ya Kaunti kulihalimisha kutoka mahali husika iwapo wakazi watashinikiza kuondolewa kwalo.

Akiongea na mwandishi huyu katika afisi kuu za bunge la Kaunti ya Mombasa siku ya Ijumaa, Suleiman Boma, alisema kuwa atafanya juhudi kumfikia waziri au gavana wa kaunti ili kutafuta njia ya kutekeleza maoni ya wakazi hao ambao wameonekana kutofurahishwa na kuwekwa kwa jaa hilo katika mahali pa makazi.

Boma alisema kuwa tatizo kubwa ambalo limekuwa ni ukosefu wa malori ya kutosha ya kuzoa taka hali ambayo imesabisha taka kurundikana mahali hapo.

“Ninatafuta njia mwafaka ya kuona kuwa taka zilizoko kwenye jaa hilo hazitakuwa hasara bali faida kwa kutafuta wawekezaji kubadilisha taka hiyo iwe ya manufaa kwa wakazi na Kaunti ya Mombasa kwa jumla,” alisema Boma.

Hata hivyo, alisema kuwa kuna baadhi ya wakazi kutoka eneo hilo la Kibuyuni ambao wanatumiwa na wapinzani wake wa siasa kuweka siasa kwenye suala hilo.

Aliwataka kuacha kufanyia masuala muhimu kama hayo siasa na badala yake kushirikiana kupata utatuzi wa masuala yanayo wakumba wakazi.