Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni Maxwell Masai, amemtaka mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko kuwafungulia mashtaka majaji na mahakimu wafisadi nchini.

Akiongea na wanahabari afisini mwake katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Masai alisema kuwa iwapo Tobiko atachukua jukumu hilo, basi kwa kiwango kikubwa idara za mahakama zitapunguza ufisadi.

Masai alisema kuwa Wakenya wanaimani na mahakama za humu nchini kwa asilimia kubwa lakini hatua ya hivi majuzi, ya Jaji wa mahakama kuu zaidi nchini Philip Tunoi, kuhusishwa katika sakata ya ufisadi imewafanya wananchi kutoamini uamuzi wa Mahakama.

Kiongozi huyo wa vijana alisema kuwa sharti Tobiko kuchukua hatua za dharura dhidi ya Jaji Tunoi na mahakimu wengine wafisadi ili kusaidia kuzuia kuangamia kwa mali ya umma na ukandamizaji wa Wakenya wanyonge mashinani.

“Kama viongozi wa vijana tunamtaka mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Kerioko Tobiko kuchukua hatua za dharura na kuwafungulia mashtaka majaji na mahakimu wafisadi, ili kuzuia Wakenya kukangamizwa na kunyanyaswa haki zao,” alisema Masai.

Kiongozi huyo wa vijina aliahidi kumuandikia barua Tobiko kulalamikia kuadhinishwa kwa sheria kali dhidi ya majaji, mahakimu na viongozi wengine wafisadi serikalini, ili kuondoa hofu iliyowajaa Wakenya kuhusu kukithiri kwa ufisadi mahakamani.