Wakazi wa Mombasa wametoa taathari kutokana na tuktuk moja inayotumika kuendeleza uhalifu katika jiji hilo nyakati za usiku.
Wakazi hao wanasema tuktuk hiyo imekuwa ikizunguka nyakati za usiku, na anayeendesha hujifanya kubeba abiria lakini baadae anawageuka.
Mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja kama Said aliambia mwandishi huyu siku ya Jumatatu kuwa kuna watu wengi waliojipata mikononi mwa tapeli huyo.
“Huyo jamaa anazunguka mjini kama wahudumu wengine lakini ukiabiri hiyo tuktuk yake anageuka na kuwa jambazi,” alisema Said.
Aidha wakazi hao wanawaomba wenzao kuendeleza msako na kuongeza kuwa wakiikamata wataipeleka katika kituo cha polisi cha Makupa mjini humo.
Visa vya wahudumu wa bodaboda na tuktuk kuhusishwa na ujambazi vimekuwepo sana mjini Mombasa, na kisa cha hivi majuzi ni mwezi mmoja uliopita ambapo jamaa mmoja wa tuktuk alikamatwa na polisi nyumbani kwake baada ya wakazi kuripoti kuwa anawaibia watu na kisha kutoroka.