Kiongozi wa vijana katika Wadi ya Marani, Kaunti ya Kisii, amewahimiza vijana wa wadi hiyo kutumia mikopo ya serikali kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Siku ya Alhamisi mjini Marani, David Omwancha alisema ikiwa vijana wanahitaji kuafikia maendeleo thabiti maishani, sharti watumie mikopo ya serikali haswa zile za hazina ya Uwezo Fund kupunguza hali ya umaskini miongoni mwao.
Omwancha aliwataka vijana wa wadi ya Marani kushiriki vikamilifu katika ujenzi wa taifa kwa kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kujinufaisha na hazina hiyo ya serikali pamoja na kuinua uchumi wa kitaifa.
Ata hivyo, alisema serikali ya kitaifa na zile za kaunti zimejitolea kustawisha maendeleo nchini ili kuafikia maendeleo dhabiti pamoja na kutimiza ruwaza ya 2030 kupitia vijana.
“Vijana wasipojitolea basi huenda ruwaza ya 2030 isiafikiwe. Naomba kila kijana aliye kwa kikundi ajaribu kila awezalo kuhakikisha uchumi wa taifa umeinuka, na kujinufaisha kibinafsi kwa kutumia mikopo ya serikali,” alisema Omwancha.
Aliongeza, “Tangu serikali kuu ianze kudhamini vijana katika vikundi, idadi kubwa ya vijana imeshuhudia maendeleo miongoni mwao kupitia biashara, ambapo kufikia sasa baadhi yao wana uwezo wa kujitegemea maishani kupitia mikopo ya serikali.”