Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amewaahidi wakazi kuwa idara ya usalama katika kaunti hiyo itahakikisha kuwa visa vya utovu wa usalama vinatokomezwa chini ya mwezi mmoja ujao.

Akizungumza kwenye kikao na wakazi katika eneo la Bakarani, kaunti ndogo la Kisauni siku ya Jumanne, Achoki aliyaonya makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao yanayodaiwa kuwahangaisha wakazi katika baadhi ya mitaa katika eneo bunge la Kisauni, kuwa serikali itayakabili kwa mujibu wa sheria.

“Tutachukua muda wa mwezi mmoja tu kuhakikisha kuwa eneo hili linakuwa salama kwa kila mmoja kutembea wakati wowote. Watu wachache hawawezi ruhusiwa kutatiza jamii nzima,” alisema Achoki.

Aidha, kamishna huyo aliwahimiza wakazi kushirikiana na idara ya usalama kwa kuyataja majina ya vijana wanachama wa makundi hayo, ili kuwapa maafisa wa polisi kazi ya raisi ya kuwatambua na kuwatia nguvuni.

Kwa muda sasa, wakazi wa maeneo ya Bakarani, Mtopanga, Mlaleo na Barsheba katika eneo bunge la Kisauni wamekuwa wakiishi kwa hofu kufutia makundi ya vijana kuwapora na kuwaibia wenyeji kwa kutumia visu na mapanga nyakati za mchana na usiku.