Idara ya polisi Mombasa imelaumiwa kwa kuwanyanyasa watumizi wa mihadarati kwa kuwakamata na kuwapiga badala ya kuwasaidia.
Inadaiwa kwamba mara nyingi watumizi wa mihadarati mjini humo hupitia dhulma nyingi mikononi mwa askari licha ya kwamba wanahitaji msaada kujinasua kutoka katika uraibu huo.
Mshirikishi wa shirika la kusaidia waathiriwa wa mihadarati la Reachout Trust, Taib Basheeib alisema kuwa hali hiyo imefanya vijana hao kupoteza imani kwamba wanaweza kujinasua.
“Ni changamoto kwa sababu wakiwakamata wanawapiga na hiyo pia inatupatia sisi kazi ngumu kwa sababu wanaingiwa na uoga na hivyo tunashindwa kuwafikia,” alsema Basheeib.
Wakati huo pia shirika hilo limesema kuwa serikali imeshindwa kuwekeza vifaa muhimu katika vituo vya kusaidia vijana hao ikiwa ni pamoja na madawa miongoni mwa mahitaji mengine.
“Wengine hujitokeza wakitaka kusaidiwa lakini hakuna dawa wala huduma zinazotolewa yaani kwa ufupi serikali haijawekeza vya kutosha,” aliongeza Basheeib.
Shirika hilo pia limesema kuwa moja kati ya sababu zinazofanya eneo la Pwani kuathirika zaidi na changamoto ya mihadarati ni kutokana na kwamba bidhaa mbalimbali huingizwa kupitia Bandari ya Mombasa huku ikiwa rahisi kwa madawa hayo kuingizwa bila kujulikana.
Maeneo ya Mombasa yanayotajwa kuathirika zaidi na janga hilo ni pamoja na Old Town, Majengo, Likoni miongoni mwa maeneo mengine.
Shirika hilo hata hivyo linahimiza serikali kutilia maanani vita dhidi ya mihadarati na kuwekeza zaidi katika vituo vya kutoa matibabu kwa kutoa dawa na vifaa vingine ili kusaidia zoezi hilo kufanyika kwa urahisi.