Share news tips with us here at Hivisasa

Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC imesema kuwa imejiandaa vyema katika uchaguzi mkuu ujao, na kuwa itahakikisha kuwa uchaguzi huo ni wa huru na haki.

Mshirikishi mkuu wa tume hiyo kanda ya Pwani kazkazini Amina Soud amesema kuwa zoezi hilo la uchaguzi limeandawa kikamilifu na maafisa wa tume hiyo wanaendelea kupata mafunzo zaidi ya kuhakikisha kuwa uchaguzi wa huru, wazi na haki utatekelezwa.

Akiongea na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Ijumaa baada ya kutembelea kituo cha usajili wa wapiga kura, cha Ganjoni, Soud alisema kuwa maafisa wa tume hiyo watakaosimamia shughuli hiyo wamepata mafunzo bora ya jinsi ya kutekeleza shughuli hiyo.

Afisa huyo wa IEBC aliwahimiza wakaazi wa eneo la Pwani kuhakikisha kuwa wanajitokeza katika vituo vya usajili wa wapiga kura, kwa kuwa muda uliosalia ni mchache mno na hakuna muda zaidi utakaoongezwa.

“Tunawaomba wakaazi wajitokezwe kwa wingi katika siku hizi zilizosalia ili wajisajili kama wapiga kura na kushiriki moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao, kwani muda huo hautaongezwa,” alisema Soud.

Wakati huo huo, aliwahakikishia wakaazi wa eneo hilo usalama dhabiti akisema kuwa idara ya usalama ikishirikiana na maafisa wa tume hiyo wamejiandaa vyema kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inafanyika vyema.

“Tunawahakikishia wakaazi wa eneo la Pwani usalama dhabiti wakati wa huu wa zoezi la usajili wa wapiga kura kwani maafisa wa usalama wanashika doria eneo nzima la Pwani ili kufanikisha zoezi hilo,” aliongoza Soud.