Share news tips with us here at Hivisasa

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Halmashauri ya Bandari nchini KPA, Catherine Wairi amesema kuwa ujenzi wa Bandari ya Lamu utaendelea kama ilivyopangwa licha ya kuwepo na changamoto za uwekezaji katika kisiwa cha Lamu.

Akiongea na wanahabari katika Bandari ya Mombasa siku ya Jumanne mjini Mombasa, Wairi alisema kuwa mipango ya kukamilisha mradi huo unaendelea ili kuafikia malengo ya uwekezaji ya ruwaza wa mwaka wa 2030.

Mkurungezi huyo alisema kuwa mradi huo utawasaidia zaidi wakaazi katika kaunti hiyo ya Lamu.

Wairi alieleza kuwa shughuli hiyo imeambatana na ile ya bandari ndogo katika kisiwa cha Shimoni eneo la Msambweni, Kaunti ya Kwale, pamoja na ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu ili kuimarisha shughuli za kibiashara pamoja na uchumi wa nchi.

Aidha, alisema kuwa shughuli za kibiashara pamoja na ukuzaji uchumi wa taifa hili utaimarika zaidi iwapo wadau mbali mbali watashirikiana na halmashauri hiyo kuafikia malengo yake ya kuingia katika bandari bora ulimwenguni, kwani tayari Bandari ya Mombasa ni kati ya bandari bora tano Afrika.

"Ujenzi wa bandari mpya ya Lamu utaendelea hadi kukamilika licha ya kuwepo na msukosuko wa uwekezaji na wakaazi wa Kisiwa cha Lamu kuhusu maswala ya fidia. Kama KPA tuna amini serikali inalishughulikia suala hilo ili kuboresha shughuli za kibiashara na uchumi pamoja na kuwasaidia wakaazi kupata ajira,” alisema Wairi.

Usimamizi wa KPA umeonekana kuchukua mkondo mpya wa uwekezaji baada ya halmashauri hiyo kufanyiwa marekebisho ya uongozi.