Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa kijiji cha Nyamwanga wana kila sababu yakutabasamu baada ya kiongozi wa eneo hilo kuwahakikishia kumaliza ujenzi wa zahanati ambao ulikuwa umesitishwa kwa ukosefu wa pesa.

Akihutubu katika zahanati ya Magombo alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, mbunge wa Kitutu Masaba, Timothy Bosire, aliagiza kamati ya hazina ya CDF katika bunge hilo kuhakikisha kuwa imepeana pesa hizo ili kusaidia kumaliza ujenzi huo.

Mbunge huyo pia aliagiza mwanakandarasi aliyekuwa akijenga zahanati hiyo kurejelea ujenzi huo mara moja.

"Kamati ya CDF imetenga Sh2.5m ili kuhakikisha kuwa ujenzi huu umekamilika kwa kipindi cha miezi mitano ijayo. Ninamwagiza mwanakandarasi aliyekuwa akijenga zahanati hii kurejelea majukumu yake kwa haraka ili kuhakikisha mradi huu umetamatika kwa wakati unaofaa," alisema Bosire.

Mbunge huyo ambaye vilevile ni mwekahazina wa kitaifa wa chama cha ODM alihaidi wakazi wa eneo hilo kuwa atahakikisha kuwa miradi yote iliyoanzishwa na mbunge wa zamani wa eneo hilo Walter Nyambato imekamilika.

"Ninajua kuwa miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wangu kabla niingie madarakani ilikuwa imetengewa pesa na kujitolea kwangu kuikamilisha haimaanishi kwamba uchunguzi hauwezi fanywa kuhusiana na kutokamilishwa kwa miradi hiyo kwa kuwa tunahitaji uwazi na uwajibikaji," alisema Bosire.

Haya yanajiri baada ya joto la kisiasa kuibuka kati ya mbunge wa sasa Timothy Bosire na mtangulizi wake Walter Nyambati kuhusiana na shtuma za utumizi mbaya wa pesa hali iliyo sababishwa ujenzi wa zahanati hiyo kustishwa.