Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imeahidi kuimarisha usalama katika fuo za bahari msimu huu wa likizo ya mwezi wa Desemba.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amesema idara tofauti za usalama ikiwemo polisi wa kawaida, wale wa utawala na maafisa kutoka shirika la huduma kwa wanyama pori nchini KWS watashirikiana kuimarisha usalama katika maeneo hayo.

Akizungumza na wanahabari mapema siku ya Jumatatu wakati wa kuzindua rasmi kituo cha kushika doria katika ufuo wa bahari wa Kenyatta jijini Mombasa, Marwa alisema kwamba wakazi sawia na watalii kutoka maeneo mbali mbali ya nchi waondoe hofu yoyote kwani usalama umeimarishwa katika maeneo yote ya fuo za bahari sawia na maeneo ya kujivinjari kama vile bustani ya Mama Ngina.

“Nataka kuwahakikishia wakazi wa Mombasa kuwa usalama umeimarishwa katika maeneo yote ya umma, kama munavyoona tuko na idara mbali mbali za usalama wakiwemo polisi wa utawala na KWS,” alisema Marwa.

Hali ya usalama katika baadhi ya maeneo ya Mombasa, haswa eneo la Kisauni ilikuwa tete kutokana na genge la wahalifu ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi, ila Kamishna huyo ameapa kukabiliana vilivyo na vikundi hivyo na kuyaangamiza.

Vile vile Marwa ameomba ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa kuhusiana na magenge hayo ili kufanikisha mikakati ya kuimarisha usalama katika Kaunti ya Mombasa na kuirudisha katika hadhi yake ya hapo kale.

Kituo hicho cha kushika doria kimezinduliwa siku chache tu baada ya mwanamume mmoja mwenye umri wa makamo anayedaiwa kuwa mmoja miongoni mwa vijana hao wa kikundi cha 'Wakali Kwanza' kuuwawa na maafisa wa polisi.