Mamlaka ya kusimamia barabara kuu nchini KeNHA imetakiwa kumwajibisha mtwanakandarasi anayekarabati barabara ya Nakuru kuelekea Subukia, kuhakikisha kwamba imetiwa alama.
Abiria wanaotumia barabara hiyo wamekuwa wakilalamikia mwendo wa kasi wa ukarabati wa barabara hiyo, ukosefu wa alama pamoja na utendakazi duni.
Hayo yanajiri baada ya magari matatu kugongana katika eneo la Ahero, kwa kile wakaazi wanasema ni ukosefu wa alama za barabarani.
“Idara ya serikali inafaa kuhakikisha nyoro anaweka alama kwa sababu karibu sasa afunganye virago, na hata matuta aliyoweka hayana ishara ya kuonyesha yamo barabarani” alisema abiria Alice Kariuki.
Na wakati uo huo KeNHA imeelezea wasi wasi wake dhidi ya ongezeko la visa vya ajali zinazohusisha wapita njia mjini Naivasha.
Kutokana na hayo, mamlaka hiyo imesema kuwa imeanzisha mpango wa kuweka vipima mwendo katika maeneo ya Kayole na Kinungi kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru.
Kuwekwa kwa vifaa hivyo kutakuwa afueni kubwa kwa wakaazi wa sehemu hizo ambao wamekuwa wakiililia serikali kutatua tatizo la ajali eneo hilo.
Takwimu za hivi punde aidha zimeonyesha kuwa angalau watu mia mbili wamepoteza maisha yao wengi wao wakiwa watoto wanaovuka barabara hiyo wakielekea shuleni mwaka huu.
Barua iliyoandikwa na meneja wa mamlaka hiyo Ezekiel Fukwo, ilisema kwamba: “kazi ya kuweka vifaa hivyo vya kupima kasi ya magari itaanza katika kipindi cha wiki moja ijayo”.
Fukwo amesema tayari mwanakandarasi mmoja amepatikana na ambaye pia atafanya ukarabati kwenye maeneo ya barabara hiyo ambayo yamechipuka.