Vijana kutoka maeneo tofauti ya kaunti za Pwani wameeleza kukumbwa na changamoto za kupata zabuni zinazotolewa na serikali, wakitaja ukosefu wa ufahamu wa kutosha wa taratibu za kupata zabuni hizo kama kikwazo.
Hii ni licha ya serikali kuweka sheria ya asilimia 30 ya zabuni zake kuelekezwa kwa makundi ya vijana na wanawake.
Kufikia sasa ni makundi machache yaliyofadaika na sheria hiyo.
Wakizungumza katika warsha ya vijana iliyoandaliwa mjini Mombasa na shirika la kimataifa la DSW siku ya Jumatano, vijana hao wametoa wito kwa taasisi husika kuwapa motisha vijana mashinani na kuwaelemisha kuhusiana na jinsi ya kupata zabuni hizo.
Wakati huo huo, mshirikishi wa miradi eneo la Pwani katika shirika la DSW George Ouma aidha ametoa wito kwa vijana kujihusisha kikamilifu katika nafasi mbali mbali zinazotolewa na serikali hususan wakati huu ambapo taifa linaelekea katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu kutoka malengo ya maendeleo ya millennia.