Mwenyekiti wa Shirika la wanawake wa kiislam nchini amesema kuna haja ya jamii kuungana na kutoitumia dini vibaya ili kudumisha amani na kuepukana na ugaidi.
Akiwahutubia viongozi mbali mbali wa dini ya kiislam, wazazi na vijana wa eneo la Pwani katika kongamano la kiusalama mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Bi Farida Rashid, alisema kwamba dini hairuhusu vijana kujiunga na ugaidi wala harakati za msimamo mikali bali inazingatia amani na umoja.
Kulingana na Bi Farida, kuna haja ya vijana kushauriwa na kutambua vyema misingi ya dini ya kiislam ili kueneza ujumbe wa amani katika jamii.
Rashid pia alisema vijana wanapswa kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa usalama katika juhudi za kuimarisha usalama nchini.
“Kuna haja ya vijana wetu kushauriwa jinsi ya kuwa na maadili mema kwani dini hairuhusu mambo ya ugaidi na misimamo mikali. Iwapo vijana watajitenga na mambo hayo, basi taifa hili na hususana eneo la Pwani litakuwa na usalama dhabiti,” alisema Rashid.
Rashid aliwataka vijana katika eneo la pwani kuzingatia ushauri wa wazazi wao na jamii kwa jumla na kujinasua kutokana na harakati za misimamo mikali na ugaidi ili taifa hili liwe na usalama dhabiti.
Matamshi ya Rashis yamejiri baada ya idara ya usalama nchini kutoa tahadhari kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi huku maafisa wa usalama wakitumwa mashinani kushika doria na kuimarisha usalama.