Vijana katika eneo la Kabete wamehimizwa kujihusisha na shughuli za kujiendeleza ili kuzuia kuingizwa katika itikadi mbovu kama ugaidi.
Jamii ya waislamu, wakiidhinisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Mohammed hii leo na ambao walikua wakizungumza katika msikiti wa Kabete waliwahimiza vijana wawe wenye bidii ya kujihusisha na miradi ya kujiendeleza, au pia bishara zao ili wasiwe rahisi kushawishiwa na makundi ya kigaidi.
Sheikh Abdul Rahim, akizungumza katika msikiti huo alisema kuwa vijana wengi wa kiislamu ambao hawana ajira ndiyo wana hatari ya kuuingizwa katika itikadi mbovu kama ugaidi kwa kuwa hawana kazi wala biashara zao.
Alisema kuwa visa hivi vinaweza isha ikiwa vijana wakipata ajira ama kuanza biashara zao.
Alisema makundi haya ya ugaidi yanategea sana vijana ambao hawana ajira kwa kuwaahidi pesa nyingi na hata kuwapa pesa ili kujiunga.
Sheikh Rahim alisisitiza kuwa kuna wazazi ambao hawatii moyo wanao wala kuwapa msaada wa kifedha kuanza biashara zao, huku akiwahimiza wazazi wawe na uhusiano mzuri na watoto wao ili kuelewa masaibu yanayowakumba.
"Dini ya kiislamu hairuhusu ugaidi, na ndiposa lazima tupigane dhidi ya itikadi hizi potovu. Tunataka vijana muwe wenye bidii ya kutafuta, mfungiwe biashara ili kujikimu kimaisha, wazazi pia ni jukumu lenu muwe waangalifu na muwashauri vijana kwa njia zinazofaa," alisema kiongozi huyo.