Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetoa wito kwa akina mama na vijana wa eneo hilo kujitokeza katika afisi za kaunti na kuwasilisha mapendekezo ya miradi yao ili kupata ufadhili.
Vijana na akina mama katika eneo hilo wamelaumiwa na serikali hiyo kwa kukosa kuungana pamoja na kujitokeza kwa kuanzisha miradi ya maendeleo.
Akihutubia wananchi katika Uwanja wa Tononoka mjini humo siku ya Jumanne, mkuu wa idara ya vijana, jinsia na michezo Mohamed Abbas alisema kuwa serikali ya kaunti imetenga fedha za miradi lakini wanawake wamezembea.
“Ikiwa wanawake muna mipango mnayojua kwamba itawasaidia, msiogope kuja katika afisi za kaunti ili tufadhili miradi yenu,” alisema Abbas.
Serikali hiyo ilisema kuwa wale waliojitokeza hapo awali tayari wameanza kufaidi huku ikiwahimiza wengine kuchukua mfano huo.
Abbas alisema kuwa takriban vijana 100 wamefaidika na ufadhili wa masomo ya kibiashara na kisha kupata vyeti kutoka chuo kikuu.
Kaunti ya Mombasa ina jumla ya wadi 30 na katika kila wadi kulichaguliwa vijana watatu huku wengine 10 wakichukuliwa kutoka katika familia maskini.
“Akina mama munafaa mjitokeze mje na miradi yenu ili tuone vile tutawafadhili nanyi mpate haya mafunzo,” aliongeza Abbas.
Abbas pia alisema kuwa kuna kumbi mbalimbali za kufanyia mikutano na kwamba kundi lolote liko huru kwenda kwa serikali hiyo kuitisha nafasi ya kufanyia mikutano.