Viongozi wanawake katika ukanda wa Pwani wamewaonya vijana na wanawake dhidi ya kutumiwa na baadhi ya wanasiasa ili kuwakuza kisiasa.
Akizungumza mjini Malindi siku ya Jumamosi, Seneta mteule katika Kaunti ya Kwale Agnes Zani, aliwataka wapiga kura huko Malindi kuwa macho kuhakikisha alama inawekwa katika chama wanachounga mkono kwenye karatasi ya kupigia kura.
Alisema kuwa hatua hiyo itazuia wizi na udanganyifu.
Mwakilishi wadi mteule katika Kaunti ya Kilifi Pricillar Zawadi, alisema ahadi zinazotolewa na baadhi ya mirengo ya siasa ni njama ya kuwahadaa ili kuwaunga mkono katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi.
Zawadi alisema baadhi ya wanasiasa walikuwa katika mstari wa mbele kupinga katiba, hivyo hawapaswi kuchaguliwa kuwa viongozi.
Aidha, amewataka wananchi katika eneo bunge la Malindi kukataa siasa kandamizi na potofu, sawia na kutokubali kuhongwa kwa minajili ya kuwachagua viongozi wasiofaa.