Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Vijana wamehimizwa kutokubali ushawishi wa kuingia katika utumizi wa dawa za kulevya, na badala yake kujikakamua kuzishinda chanamoto zinazowakabili.

Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa shirika la Junior Star Mariam Mpata, aliyekuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika kongamano la vijana liliondaliwa na shirika hilo katika shule ya Oshwal, mjini Mombasa.

Takribani vijana 250 walio na umri kati ya 14 hadi 20 kutoka maeneo tofauti ya Kaunti ya Mombasa walihudhuria kuhamasishwa dhidi ya dawa za kulevya, mimba za mapema, mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa na kuwa na malengo maishani ili watimize ndoto zao.

Vijana hao walisema kuwa wamepata majibu ya maswali ambayo huwa ni nadra wazazi wao kuwaambia kutokana na taasubi na tamaduni.

Eneo la pwani lina idadi kubwa ya vijana ambao wanajihisisha na madawa ya kulevya, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limewapa viongozi na mashirika ya kujamii changamoto.