Mwenyekiti wa maktaba nchini Samuel Nyangeso amewaomba viongozi wa Kaunti ya Kisii kuacha kufanya ziara kila wakati na kuleta maendeleo kwa wakaazi.
Nyangeso alisema viongozi wengi wa kaunti hupenda kufanya ziara na wamesahau kuleta maendeleo jinsi inavyostahili.
Aliomba viongozi wa kaunti kuungana pamoja na kuleta maendeleo yale waliyowahidi wakaazi walipokua wakitafuta kura.
Nyangeso alisema ziara nyingi hazina manufaa kwa wakaazi ila wanachokihitaji ni maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumapili katika uwanja wa Nyatieko, eneo bunge la Kitutu Chache Kusini, Nyangeso alisema wakaazi wa kaunti ya Kisii wanahitaji kufanyiwa maendeleo wala si ziara za hapa na pale ambazo hazileti manufaa kwa kaunti hiyo.
“Nomba viongozi wote wa kaunti ya Kisii muungane pamoja na kuleta maendeleo. Wakazi wa kaunti hii wanahitaji maendeleo wala sio viongozi wanaoenda ziara kila wakati,” alisema Nyangeso.
Aliongeza, “Ziara ambazo mnazifanya kila mara za kutembea Nairobi na nchi za nje si za maendeleo. Naomba muungalie na kujali maslahi ya wapiga kura wa kaunti ya Kisii.”
Matamshi yake yaliungwa mkono na mwanasiasa kutoka eneo bunge la Borabu, Dkt Yobesh Kambi, ambaye alisema viongozi wanapaswa kuwajibika kwa kuleta maendeleo.