Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa dini nchini wametajwa kama watu wenye ushawishi mkubwa hasa wakati huu taifa linapokaribia kufanya uchaguzi mkuu.

Wito umetolewa kwa viongozi hao kujizatiti na kuhakikisha kuwa wanapitisha jumbe za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwachagua viongozi wenye maadili mema ili tuwe na taifa imara na lenye maendeleo.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Alhamisi, askofu mkuu katika jimbo la Mombasa Martin Kivuva alisema kuwa taifa limekuwa na changamoto nyingi ambapo viongozi wa dini wanaweza kuchangia kuleta mabadiliko.

“Tukichagua viongozi wabaya sisi wenyewe ndio tunaumia, kwa hivyo lazima tuzingatie maadili mema kila tunapofanya uamuzi,” alisema Kivuva.

Aidha, Askofu Kivuva aliwahimiza viongozi wenzake wa dini kuchukua fursa na kuhamasisha umma kuhusu maswala ya kisiasa na jinsi ya kuchagua viongozi wanaofaa.

“Kama viongozi wa dini tuna majukumu ya kuwahimiza wenzetu waangalie kwa uangalifu sana yule wanayemchagua kuwaongoza,” alisema Kivuva.

Kauli hii inakuja huku kukiwa na kashfa dhidi ya viongozi wa dini kwamba wamekuwa wakiingilia maswala ya kisiasa jambo linaloonekana kuwa kinyume na maadili ya dini.