Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu mtaani Kibera wamepongeza ziara ya papa Francis nchini huku wakisema kwamba ujumbe alio nao kuhusu amani una manufaa kwa taifa zima licha ya tofauti za kidini.

Sheikh wa msikiti wa Al Aq Sa ulioko eneo la Karanja, Suleiman Musa ni miongoni mwa waliomshukuru Papa kwa kutembelea Kenya miongoni mwa mataifa mengine ya Afrika.

Alisema majanga yanayowakumba wananchi wote yakiwemo ufisadi, yanastahili kuzungumziwa pasi na kuzingatiwa tofauti hizo za kidini.

"Madhumuni ya ziara ya Papa Francis Nchini Kenya ni kuleta ujumbe wa amani na kuzungumzia maswala mengine hasa ufisadi ambao kwa sasa umekita mizizi. 

Hatua hii pia inatukumbusha kwamba tunastahili kuishi kwa umoja na utangamano licha ya tofauti zetu za kidini," alisema Suleiman.

Sheikh huyo aliyasema haya siku ya Jumatano kwenye mahojiano ya kipekee na ripota huyu katika msikiti huo wa Al Aq Sa. Alitoa wito kwa jamii ya Kiisalmu kumkaribisha kiongozi huyo maarufu kote duniani katika dhehebu ya kikatoliki.

"Hakuna tatizo lolote kwa waislamu kumkaribisha Papa kwa msingi wa anayokuja kuwasilisha nchini. Umoja wetu kama taifa ni wa manufaa," aliongeza Sheikh Musa.