Viongozi wa chama cha TNA katika kaunti ya Kisii na Nyamira wamesema kuvunjwa kwa vyama vya TNA na URP ni kunyima wananchi uhuru na haki wa kutumia vyama mbalimbali katika siasa za nchi.
Kulingana na viongozi hao walisema wananchi hawakuhusishwa katika hatua hiyo ya kuvunja vyama na kuingia katika chama kimoja cha Jubilee party kama inavyohitajika kikatiba. Walisema hatua hiyo inakiuka katiba.
Wakizungumnza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Kisii, mwenyekiti wa chama cha TNA katika kaunti ya Kisii Naftal Obare na mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti ya Nyamira Joel Bikundo walisema kuvunjwa kwa vyama tanzu na kujiunga katika chama kimoja inaenda kinyume na demokrasia.
“Hatutakubali vyama vyetu kuvunjwa kwa sababu hiyo ni kurudisha nchi yetu nyuma na kunyima wakenya haki yao. Sisi tunahitaji democrasia ya nchi iendelee mbele na hatutarudi nyuma,” alisema Naftal Obare
Sasa viongozi hao wamesimama kidete na kusema hawatakubali vyama vya TNA ,URP na vingine kuvunjwa hadi sababu halisi itolewe na wananchi wahusishwe kwa kutoa maoni yao kabla ya hilo kulikubalia kuendelea
“Sisi tutaendelea kusalia kuwa katika vyama vyetu hayo mengine ya Rais na viongozi wengine hatuyajui," Joel Bikundo.
"Hapa Kisii tunamwambia Rais Uhuru Kenyatta hatujakubali hayo ya kuvunja vyama tanzu ,” aliongeza.