Mshauri wa maswala ya uandishi habari hapa nchini Vitalis Musebe amesema huenda taifa likakwama kimaendeleo ikiwa wanasiasa wanaotoa matashi ya chuki hawatachukuliwa hatua.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Musebe alisema kuwa matamshi hayo huenda yakawatia hofu baadhi ya wawekezaji humu nchini na kupelekea wageni kususia kuzuru Kenya.
Musebe alisema kuwa matamshi hayo hudhoofisha umoja na utangamano wa taifa.
“Taasisi zilizotwikwa wajibu wa kuhakikisha kuna utangamano na uwiano nchini kama vile NCIC miongoni mwa taasisi zingine, sharti zionyeshe makali yake kwa kuwachukulia hatua kali watuhumiwa,” alisema Musembe.
Aidha, ametoa wito kwa waandishi wa habari kutokimya na badala yake waangazie kikamilifu viongozi hao ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watu wenye nia ya kuwagonganisha wananchi.
Wananchi pia wametakiwa kutoshabikia matamshi hayo na badala yake kuasi viongozi wachochezi.