Viongozi katika Kaunti ya Nakuru wametakiwa kushirikiana na vyombo vya habari kwa mustakabali wa kaunti na taifa kwa jumla.
Akizungumza siku ya Jumatano wakati wa kikao na wanahabari mjini Nakuru, mwanaharakati Masese Kemunche kutoka shirika la Centre for Enhancing Democracy and Good Governance (CEDGG) alisema kuwa katiba ya sasa ilipiganiwa na inafaa kulindwa.
Aidha, mwanaharakati huyo alisema kuwa si jambo la busara kwa viongozi kujaribu kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
"Wanahabari wana wajibu wao na uhuru wa kikatiba na hawafai kudhulumiwa au kunyimwa haki zao," alisema Kemunche.
Wakati huo huo, Kemunche alitoa wito kwa vyombo vya habari kutokubali kukandamizwa na baadhi ya viongozi ambao alitaja kama maadui wa maendeleo na katiba mpya.
"Wanahabari hamfai kukandamizwa kwasababu muna uhuru wenu wa kikatiba," alisema Kemumche.
Matamshi sawia yalitolewa na mwanaharakati mwenzake Joseph Omondi, ambaye alisema kuwa jamii pasina vyombo vya habari ni giza tororo.
Wawili hao pia walitoa wito kwa wanahabari na viongozi kuungana kudumisha Amani nchini.