Mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Mombasa Afiya Rama amewasuta viongozi wakisiasa wanawake katika Kaunti hiyo, kwa kile amekitaja kama kuwasahau wanawake wenzao pindi wanapochaguliwa katika viti vya kisiasa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Bi Rama alisema kuwa viongozi hao wamefeli kutetea haki za wamama licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kuwasilisha na kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakumba akina mama mashinani zinaangaziwa na kutatuliwa.
“Hawa wanawake wenzangu wametufeli. Wakishapigiwa kura wanageuka na kuwa kama wanaume. Hawajali matatizo yanayowakumba wenzao hapa vijijini,” alisema Rama.
Mtetezi huyo wa haki za wanawake sasa amewataka viongozi hao kuzuru mashinani na kuandaa mkutano na wanawake ili kupata maoni yao katika hatua itakayohakikisha kuwa sauti za akina mama zinaangaziwa wakati wa kutoa maamuzi kuhusu baadhi ya masuala yanayowahusu.
Bi Rama aidha, aliwahimiza akina mama kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao ili waweze kujihakikishia nafasi katika uongozi nchini.