Kufuatia mauaji ya mfanyabiashara mmoja katika eneo la Kisauni jana Jumanne, wakazi kutoka mtaa huo wamewataka viongozi na maafisa wa idara ya usalama kuungana na kukabili jinamizi la ukosefu wa usalama katika kaunti hiyo.
Wakiongea na mwandishi huyu jiji Mombasa kupitia mzee wa mtaa Ali Abdi, wakazi hao walisema ni vyema viongozi wote wa ngazi zote kushirikiana na idara inayoshughulikia masuala ya usalama kutafuta suluhu la mapema ili kuzuia na kuepusha wanainchi kuendelea kuuliwa na majambaji bila sababu kwa kuwa kila mmoja ana haki ya kuishi.
Bw Abdi alisema wakati umefika hata wakazi kuanza kufanya mikutano ya kuhubiri umuhimu wa kukaa kama ndugu na dada na kuwashauri hasa vijana ambao wengi hawana kazi njia mwafaka ya kupata riziki yao badala ya kujihusisha katika uhalifu.
“Sisi kama wakazi pia tuna wajibu wa kuwaweka vijana na jamii kwa jumla kwenye vikao na kuwapa mwelekeo mwafaka jinsi ya kutangamana na kuweka usalama badala ya kudhoofisha usalama wa jamii na hiyo ni kinyume na sheria na mara nyingi wakipatikana na mkono wa sheria watauliwa,” alisema mzee Abdi.
Wito wake unakuja huku Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan akiitaka idara ya usalama kuwajibika vilivyo wanapofanya wajibu wa kulinda umma katika Kaunti hiyo.