Share news tips with us here at Hivisasa

Baraza la Maimamu na Wahubiri humu nchini (CIPK) limetoa mwito kwa viongozi wa kisiasa kujitenga na matamshi ya chuki na uchochezi wanapohudhuria ibada za Jumapili Kanisani.

Akiongea na wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne, Katibu Mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa alisema viongozi wa kisiasa wamekuwa wakichukua fursa hiyo ya ibada za Jumapili kuwashambulia baadhi ya viongozi serikalini wanaokabiliwa na kashfa za ufisadi.

Kulingana na Sheikh Khalifa hatua hiyo inalenga kuwagawanya wakenya kwa misingi ya kisiasa na kidini na inastahili kukomeshwa mara moja ili kuzuia kushughudiwa kwa mafarakano nchini.

Sheikh Khalifa alisema maeneo ya kuabudu yanafaa kupewa heshima kulingana na mafunzo ya dini ya Kikristu na Kiislam na akawataka viongozi hao wa kisiasa kushiriki ibada makanisani na kuondoka kwa amani ili kuzuia kutowagawanya wakenya.

"Tunawaambia viongozi wa kisiasa kukoma kutumia majukwaa ya ibada wanapohudhuria ibada za Jumapili na kutoa matamshi ya chuki kwani hatua hiyo huenda ikachangia migawanyiko miongoni mwa wakenya," alisema Sheikh Khalifa.

Matamshi ya kiongozi huyo wa kidini yanajiri baada ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kushughudiwa wakitoa matamshi ya chuki na uchochezi katika ibada za Jumapili makanisani na mikutano ya hadhara.