Mwakilishi wa wadi ya Sensi amewaomba wanasiasa kuasi siasa za kuwapotosha wananchi.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne mjini Kisii, Onchong’a Nyagaka alisema kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanaendesha siasa za kuwakosoa viongozi kwa kusema kuwa hawajafanya maendeleo.
Alisema kuwa siasa hizo zinawapotosha wananchi na kuwaomba wanasiasa hao kuwapa viongozi wakati wa kufanya maendeleo.
Onchong’a alisema kuwa kuna wanasiasa ambao kazi yao ni kukosoa viongozi bila kuleta maendeleo, na kuomba wananchi kutoyafuata yale wanasiasa hao wanayoyasema.
“Naomba wanasiasa wote kujitenga na siasa na kuwapa viongozi wakati wa kufanya maendeleo. Wale ambao wanawakosoa viongozi kwenye sherehe za mazishi na katika mikutano mingine wana nia ya kuwapotosha wananchi,” alisema Nyagaka.
Aliongeza, “Kila kiongozi anajua yale anayoyafanya kama kiongozi, lakini haya mengine ya kulaumu viongozi si njia bora kwani wengi hudanganya wananchi,” alisema Nyagaka.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo aliahidi kufanya maendeleo mengi katika wadi yake, kama vile kukarabati barabara za Chimo-Engoto, Marani-Nyakenogo, Riatambo-Sombogo, pamoja na barabara ya Itare-Riakerongo.
Aidha, mwakilishi huyo alisema atajaribu kila awezalo kuhakikisha miradi ya maji imewekwa katika kila sehemu ya wadi yake, ili kuwafaidi wakaazi kwani idadi kubwa ya akina mama husumbuka kutafuta maji kwa kutembea masafa marefu.