Vyama 151 katika eneo bunge la Nyaribari Masaba kaunti ya Kisii vimepokezwa mikopo kutoka katika hazina ya Uwezo fund ili kuanzisha biashara za kujiimarisha kimaisha na kuinua uchumi wa kaunti na taifa.
Miongoni mwa vikundi ambavyo vilipokezwa pesa hizo ni vikundi vya vijana, akina mama na walemavu.
Akizungumza mnamo siku ya Jumatatu wakati vikundi hivyo vilipokezwa pesa hizo katika eneo bunge hilo mwenyekiti wa hazina hiyo katika eneo hilo Dennis Ongori alisema pesa ambazo hazina hiyo ilipokeza vikundi hivyo ni millioni 8.2 huku vikundi hivyo vikipata kati ya shillingi 50,000 na 80,000.
“Katika eneo bunge letu la Nyaribari Masaba hazina ya Uwezo ita nufaisha wakaazi wengi kwa kuwawezesha kujiendeleza kupitia biashara,” alisema Ongori.
Wakati huo huo, Ongori aliomba kila kikundi kujaribu kila liwezavyo kuhakikisha wametumia pesa vizuri na kupata faida ili kujiendeleza.
“Kila kikundi lazima kitumie pesa vizuri maana pesa hizo ambazo tunawapa mtatakiwa muzirudishe baadaye, kabla ya kurudisha nanyi pia sharti muhakikishe mumepata faida kutoka kwa pesa hizo,” aliongeza Ongori.