Share news tips with us here at Hivisasa

Waathiriwa wa ghasia za baada ya uchuguzi wa mwaka 2007 katika eneo la Kisii, wakiongozwa na mwenyekiti wao Alfred Akama, wamesema wanabaguliwa zaidi kielimu na afisi zingine za serikali.

Kulingana na mwenyekiti huyo, wanapofuata pesa za basari ili kuwaendeleza wanao kielimu katika afisi za serikali, wanabaguliwa vikali kwa kudaiwa si wenyeji wa maeneo wanapoenda kufuata pesa hizo ili kuwasomesha watoto wao.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, Akama alisema waathiriwa hao wameonekana kudhulumiwa na kubaguliwa hadi kupita kiasi, na kuomba serikali kuwafidia ili kutafuta mahala pa kuishi bora kuwe na amani.

Aidha alisema baadhi yao wanapojiandikisha kupata vitambulisho hufukuzwa kwa kutojulikana, huku wakiomba serikali kiuingilia kati ili kuwaokoa kutoka mtego wa aina hiyo.

“Tumekuwa tukibaguliwa katika afisi za serikali, hata machifu wanatuambia hatujulikani tunapoenda kutafuta msaada wa usaidizi ili watoto wetu waendelee na masomo,” alisema Akama

“Kuna wengine wanafuatilia vitambulisho baada ya kufikisha miaka 18, nao wanabaguliwa vikali mpaka tumeshindwa pa kuenda, tufanye nini kama serikali haitaki kutusaidia? aliuliza Vincent Nyachachi, mmoja wa waathiriwa.

Sasa wito huo wa waathiriwa hao wa ghasia za mwaka wa 2007 hadi mwaka 2008 wanaitaka serikali kuwafidia ili kutafuta mahala pa kuishi .

"Tunaomba serikali itufidie pesa kama kabila zingine ambazo tayari zimefidiwa,” alisema Nyachachi.