Baadhi ya wabunge wa kitaifa kutoka kaunti ya Nyamira wamejitokeza kushtumu mbinu zinazotumika na tume ya kukabili ufisadi nchini EACC kukabiliana na visa vya ufisadi.
Wakiongozwa na mbunge wa Mugirango magharibi Charles Geni, wabunge hao waliishtumu tume ya EACC kwa kutokuwa huru wakati wa kuchunguza visa vya ufisadi huku wakisisitiza kuwa yafaa tume hiyo ingolewe mamlakani.
"Tume ya kukabili visa vya ufisadi nchini EACC imewafeli wakenya na ningependa kuwahakikishia kuwa mswada niliouandaa ili kuibandua tume hii ofisini uko karibu kutamatika na ninatumai kuwa wabunge wenzangu wataniunga mkono kwa maana tumechoshwa na tume inayothibitiwa na watu fisadi," alisema Geni.
Kwa upande wake mwakilishi wa kina mama katika kaunti hiyo Alice Chae alishangazwa na ni vipi tume ya EACC inavyoshughulikia kesi ya aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru, huku akiitaja tume hiyo kama fisadi.
"Nitakuwa wa kwanza kuunga mkono mswada huo wa kutokuwa na imani na tume ya EACC kwa maana tume hiyo inapalilia ufisadi nchini kwa maana hadi sasa hatujaelewa jinsi ilivyomwachilia waziri Waiguru kuhusiana na shtuma za ufisadi zinazokabili shirika la vijana nchini NYS," alihoji Chae.