Wafanyikazi katika machimbo ya mawe eneo la Katine, katika kaunti ndogo ya Matungulu wamelalamikia ukosefu wa kazi baada ya machimbo hayo kujaa maji.
Wafanyikazi hao walisema kuwa biashara ya mawe imelemazwa katika eneo hilo kufuatia mvua ya El Nino inayoshuhudiwa nchini.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano, wachimba mawe hao walisema wamelazimika kutafuta kazi zingine ili kuweza kukidhi familia zao baada ya machimbo hayo kujaa maji.
"Biashara yetu hunoga mno hasa wakati wa kiangazi. Ingawa mvua ni baraka, imelemaza kazi yetu ya uchimbaji mawe na kutulazimu kusaka kazi sehemu zingine ili tuweze kulisha familia zinazotutegemea,” alisema Cyrus Kyatha, mchimba mawe.
Vilevile, wakazi katika eneo hilo waliomba machimbo hayo kuwekewa ua ili kuzuia watoto wadogo kutumbukia ndani yanapofurika hasa wakati huu wa likizo.
Esther Waeni, mkazi wa Katine, alisema kuwa machimbo mengi yapo njiani na hivyo in hatari hasa wakati was usiku kunapokuwa na giza totoro.
"Machimbo haya ambayo ni ya vina virefu huenda yakaleta madhara wakati huu wa mvua ambapo watoto wachanga huenda wakatumbukia ndani,” alisema Waeni.