Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa waendeshaji wa pikipiki eneo la Kongowea umetishia kufanya maandamano kupinga vikali pendekezo la kuongezwa kwa bei ya pikipiki nchini.

Akizungumza na mwanahabari huyu siku Alhamisi, mwenyekiti wa chama cha bodaboda wa Kongowea eneo bunge la Nyali, Samuel Ogutu alisema mswada huo unakandamiza maisha ya waendesha bodaboda na mwananchi wa kawaida, ikizingatiwa hiyo ndio ajira pekee ambayo iko na idadi kubwa ya vijana.

Ogutu aliongeza kuwa vijana wengi watapoteza ajira na mwishowe kujihusisha na uahalifu utakaopelekea kudorora kwa usalama katika jamii.

Aidha, aliwasihi wabunge kufutilia mbali mswada huo mara moja ili kutoa hofu kwa wamiliki na waendeshaji wa pikipiki.

Haya yanajiri baada ya bunge kuidhinisha mapendekezo ya raisi Uhuru Kenyatta, siku ya Alhamisi ya kutaka bei ya pikipiki, vinywaji vya matunda na magari kupanda bei kwa asilimia kumi.

Siku ya Alhamisi wabunge wa mrengo wa Jubilee walipitisha mapendekezo hayo licha ya wenzao wa upinzani kuondoka bungeni wakipinga mapendekezo ya rais Uhuru wakisema yataongeza zaidi mzigo wa gharama ya maisha kwa mwananchi.

Kwa sasa anayetaka kununua pikipiki atalazimika kuongeza shilingi elfu zaidi ya bei iliyoko dukani, mwenye kununua gari lililotumika chini ya miaka miwili atalazimika kuongeza shilingi laki moja unusu na yaliyotumika zaidi ya miaka mitatu ataongeza shilingi laki mbili.

Kwa kinywaji chochote cha matunda itaongezeka shilingi kumi kwa kila lita.