Waendeshaji bodaboda mjini Nakuru wametakiwa kulipa mikopo waliopokea kutoka kwa vyama vya ushirika mjini Nakuru.
Mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda mjini Nakuru Simon Ongoro amesema kuwa wengi wa wahudumu wa bodaboda walionufaika na mikopo hiyo wanakwepa kuilipa ama wanachelewa kufanya hivyo.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Nakuru, Ongoro alisema kuwa mashirika mengi ya kukopesha fedha na vyama vya ushirika vimewasilisha malalamishi kwa ofisi yake kuhusu vijana ambao wamedinda kulipa mikopo.
“Kuna wahudumu wa bodaboda ambao walipokea pesa fulani kutoka kwa vyama na wakakubali kulipa baada ya muda fulani, lakini tunapozungumza, wengine hata hawajulikani walipo na wengi wamekataa kulipa pesa hizo,” alisema Ongoro.
Aliongeza, “ Ofisi yangu imepokea malalamishi hayo na tunawataka wahudumu wa bodaboda walionufaika na mikopo hiyo kuwa watu wema na kuilipa ili wengine wafaidike nayo pia.”
Ongoro alisema kuwa iwapo vijana hao hawatapatikana, basi muungano huo utalazimika kugharamia mikopo hiyo kwa kuwa ulitoa dhamana wakati wa kupeanwa kwake.
“Sisi ndio tuliwadhamini na iwapo watakosa kulipa fedha hizo, sisi ndio tutalazimika kuwalipia lakini tutawatafuta na kuhakikisha kuwa wamelipa mikopo hiyo,” alisema Ongoro.
Aidha, alionya kuwa huenda mashirika ya kifedha yakahofia kuwapa mikopo waendeshaji bodaboda iwapo tabia hiyo ya kukwepa kulipa itaendelea.
Mikopo hiyo ilitolewa kwa vijana kununua pikipiki na kufungua biashara ndogondogo kama njia ya kujikimu kimaisha.