Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa muungano wa wahudumu wa hoteli na wapishi nchini tawi la Mombasa Sam Ikwaye, amewapongeza wafanyibiashara ambao wamewekeza katika sekta ya hoteli mjini humo.

Ikwaye alitaja hatua hiyo kama itakayochangia pakubwa kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu wakati wa kuzinduliwa kwa hoteli mpya ya Pride Inn Paradise Beach Resort na Sun Africa Beach Resort, Ikwaye alisema kuwa kujengwa kwa hoteli zaidi kunaashiria kuwa idadi ya wageni wanaozuru mjini humo inazidi kuongezeka.

“Nataka kuwapongeza wawekezaji wanaozidi kupanua sekta ya utalii nchini kwa kujenga hoteli za kisasa. Hii ni ishara tosha kuwa tunapiga hatua,” alisema Ikwaye.

Kulingana na Ikwaye, miaka ya hivi majuzi eneo la Pwani hususan Mombasa imekuwa ikishuhudia hoteli nyingi zikifungwa huku wamiliki wakizigeuza maeneo ya kufanyia biashara nyingine kufuatia kushuka kwa mapato.

Hata hivyo, kwa sasa hali hiyo imeripotiwa kubadilika kwani wengi wamezamia biashara ya hoteli kutokana na ongezeko la wageni wanaoutembelea mji wa Mombasa.

Kwa upande wake, meneja wa hoteli ya Pride Inn Paradise Resort, Imtyaz Mirza, alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo kumeziba pengo katika sekta ya utalii ambalo limekuwa kwa muda sasa.

Mji wa Mombasa ulishuhudia wageni wengi katika msimu wa Krismasi na mwaka mpya jambo ambalo lilitajwa kuchangiwa na kuimarika kwa usalama nchini.