Huku uchaguzi wa wawakilishi wa chama cha wafanyikazi wa umma nchini, ukitarajiwa kufanyika tarehe Machi 11 mwaka huu, wafanyikazi wa umma katika Kaunti ya Mombasa wameombwa kujitokeza kwa wingi ili kuwachagua viongozi waadilifu.
Katika kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Katibu mtendaji wa chama hicho Kaunti ya Mombasa Benedet Koki aliwashauri viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo kuwajibikia majukumu yao vyema.
Aidha, aliwahimiza wakazi wa Kaunti ya Mombasa hususan wafanyikazi wa umma kutopuuza uchaguzi huo kwa manufaa yao ya baadaye na kujitokeza kwa wingi ili kubadili uongozi wa chama hicho.
"Tunawaomba wafanyikazi wa umma Mombasa wasidharau uchaguzi huu wa wawakilishi wa chama cha wafanyikazi ili kuwachagua viongozi waadilifu na kutetea maslahi ya wafanyikazi kote nchini,” alisema Koki.
Kauli yake inajiri baada ya lalama kushuhudiwa kutoka kwa wafanyikazi wa umma wakilalamikia kuwepo kwa huduma duni katika Hazina ya kitaifa ya matibabu NHIF licha ya wao kutozwa ada kubwa kila mwezi.