Wahudumu wa matatu katika barabara ya Kilgoris-Kisii wameapa kutolipa ushuru kwa madai ya kulaghaiwa na askari wa kaunti ya Kisii kila siku katika barabara hiyo.
Kulingana na wahudumu hao wamekuwa wakisumbuliwa na askari wa kaunti kwa kuwalipisha ushuru wa juu zaidi huku wakidai kulaghaiwa ili kuruhusiwa kupita jambo ambalo sasa limezua taharuki na kutaka gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae kuingilia kati kulizungumzia ili kupata suluhu halisi.
Wakizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Amariba, wahudumu hao waliandamana kulalamikia utata huo wahudumu hao wakiongozwa na mwenyekiti wa wamiliki wa magari yanayohudumu katika barabara hiyo Bonface Nyang’au alisema hawatalipa ushuru hadi gavana azungumzie swala hilo la kulaghaiwa na hulipa ushuru kila siku.
“Huwa tunalipa ushuru na ushuru huo hukusanywa zaidi ya mara nne katika barabara hii na ni ya juu zaidi, wakati tunapofika eneo la Mashauri mjini Kisii askari wa kaunti huwa wanatuitisha shillingi 200 ili kuturuhusu kupita huo ni ulaghai mkubwa,” alisema Bonface Nyang’au.
“Hatutalipa ushuru wowote hadi gavana wa kaunti yetu James Ongwae azungumzie hilo halafu tuanze kulipa ushuru lakini kwa sasa hatutalipa ushuru wowote,” aliongeza Nyang’au.