Aliyekuwa waziri wa ugatuzi, Anne Waiguru, siku ya Jumatatu alitangaza rasmi azma yake ya kutaka kukiwania kiti cha ugavana, Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2017.
Waiguru ambaye kwa siku za hivi majuzi alithibitisha kuwa anataka kuugombea wadhifa wa ugavana wa Nairobi, aliiweka wazi nia yake katika mkutano wa mrengo wa Jubilee uliofanyika katika hoteli moja iliyoko karibu na barabara ya Thika.
‘‘Niko tayari kupambana na wengine wenye nia ya kuuongoza mji wa Nairobi na najua naweza,’’ alisema Waiguru.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya waziri huyo wa zamani kukiri kuwa alitafuta ushauri kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta kabla kuamua kukiwania kiti hicho.
Hata hivyo, Waiguru atakumbana na upinzani mkali kutoka gavana wa sasa, Evans Kidero, mwenyekiti wa chama cha TNA, Johnson Kiti, seneta wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, aliyekuwa mshauri wa kinara wa CORD Raila Odinga, Miguna Miguna, pamoja na aliyekuwa mbunge wa Starehe, Bishop Margaret Wanjiru.