Wakaazi wa maeneo ambayo yameripotiwa kuathirika na visa vya utovu wa usalama mjini Mombasa wamesema kuwa wanaogopa kuyataja majina ya vijana wanaotekeleza uhuni huo kwa kuhofia usalama wao.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Bakarani eneo bunge la Kisauni, wengi wao ambao ni akina mama na wazee walikiri kuyatambua magenge yanayowahangaisha wananchi.
Wakaazi hao walisema kuwa wanaogopa kutoa ripoti kwa idara ya polisi hadi watakapohakikishiwa usalama wa kutosha.
Mmoja wao aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa, alisimulia kisa ambapo mwenzake aliyetoa taarifa kwa maafisa wa polisi kuhusu makundi ya uhalifu katika eneo hilo, alivyovamiwa na vijana hao siku chache tu baada ya kushirikiana na idara ya usalama.
“Tunaambiwa tuwataje vijana hao lakini wanaachiliwa huru siku chache baada ya kukamatwa na kuja kuwashambulia waliotoa ripoti hiyo. Tutasalia kimya hadi tuhakikishiwe usalama wetu,” alisema jamaa huyo.
Siku ya Jumanne, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki aliwahimiza wakaazi kushirikiana na idara ya usalama ili kutokomeza uhalifu wa mara kwa mara katika eneo la Kisauni.
Kauli ya Achoki inajiri wiki moja tu baada ya katibu mtendaji wa Baraza la Maimam nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, kuwataka wazazi kuyawasilisha majina ya vijana wanachama wa makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao kwa maafisa wa polisi.