Wakaazi wa kijiji cha Kipata Uso huko Miritini wamesema huenda kuna ufisadi unaoendelea katika zoezi la kupewa fidia na kampuni ya ujenzi wa reli mpya ya SGR.
Wakaazi hao wanaotaka kupewa fidia ya makaburi yaliyoko katika eneo linalotarajiwa kubomolewa wanadai kampuni hiyo haijatoa mwelekeo mwafaka licha ya kufanya msururu wa vikao nao.
Katika kikao siku ya Ijumaa, maafisa kutoka katika kampuni hiyo walisema kuwa fidia hiyo inafaa kutolewa na serikali huku wakisisitiza kuwa wanataka kuendelea na ujenzi mara moja.
Akiongea na mwandishi huyu wakati wa kikao hicho, Roki Ngalaa afisa wa mawasiliano katika kampuni hiyo ya SGR alisema kuwa serikali ndio inayofaa kuwalipa wakaazi hao.
“Sisi tunataka kuanza kazi yetu mara moja lakini tunazuiliwa na wenyeji na tukiwaambia tuwape pesa kidogo tuendelee wakisubiri zingine hawataki,” alisema afisa huyo.
Kwa upande wao, wakaazi hao walisema hawatakubali kunyanyaswa na kampuni hiyo na kuongeza kuwa watazuia shughuli zozote za ujenzi eneo hilo hadi pale watakapofidia makaburi yao.
Afisa wa kushughulikia dharura kwenye shirika la kutetea haki za binadamu Muhuri Kelly Aduo akiongea na mwandishi huyu baada ya kikao hicho alisema kuwa watapeleka swala hilo kwa tume ya ardhi nchini.
“Nimeskiza huu mzozo baina ya wakaazi na usimamizi wa kampuni hii na sisi kama shirika tumeamua kufanya kikao na mwenyekiti wa tume ya ardhi Mohamed Swazuri Jumapili hii,” alisema Aduo.
Hata hivyo, afisa huyo wa Muhuri aliongeza kuwa wana wasiwasi huenda pesa hizo zilitolewa kama fidia ili zipewe wakaazi lakini baadhi ya watu wakazitumia vibaya.
Baadhi ya wakaazi waliozungumza na mwandishi huyu walielezea imani yao kwa shirika hilo la Muhuri ambalo limeonyesha nia ya kuwasaidia kupata haki.
“Tuliamua kuita shirika hili la kutetea haki za binadamu ili watusaidie kupata fidia yetu. Tuna matumaini kwamba wataleta suluhu baada ya kukutana na Swazuri,” alisema mkaazi mmoja.