Kuteuliwa kwa aliyekuwa kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kuwa mratibu wa Ukanda wa Pwani kumeungwa mkono na wananchi wengi.
Katika mahojiano na mwandishi siku ya Alhamisi, wafanyibiashara katika Soko la Kongowea, wakiongozwa na Joseph Murage, walisema kuwa Marwa ana uzoefu wa kutosha kutekeleza majukumu yake ikitiliwa maanani jinsi anavyoshughulikia swala la ugaidi.
Aidha, wafanyibiashara hao walisema kuwa Marwa ni kiongozi mwenye msimamo dhabiti na anayejiamini katika utendakazi wake.
Wafanyibiashara hao walimtaja Marwa kama kiongozi mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiusalama, katika eneo nzima la Pwani.
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Waziri wa Usalama wa Ndani na Uratibu wa Taifa Joseph Nkasseiry siku ya Jumanne, Nelson Marwa aliteuliwa kuwa mratibu mkuu wa Ukanda wa Pwani na kuchukua nafasi ya Samuel Kilele ambaye amehamishwa hadi eneo la Magharibi mwa Kenya.
Aliyekuwa mratibu wa eneo la Magharibi mwa Kenya James Ole Serian naye alihamishwa hadi jijini Nairobi.
Eneo la bonde la ufa limegawanya katika maeneo mawili, eneo la Kusini litakaloongozwa na Wanyama Musiambo, makao yake makuu yakiwa mjini Nakuru, huku Kaskazini mwa bonde la ufa kukiongozwa na aliyekuwa katibu katika Wizara ya Usalama Joseph Irungu.
Aidha Claire Omollo aliyekuwa mratibu wa Mashariki mwa Kenya, Osman Warfa aliyekuwa akihudumu bonde la ufa, Njoroge Ndirangu wa Nairobi na Francis Mutie wa Nyanza, wamehamishwa hadi jumba la Harambee jijini Nairobi.
Hatua hiyo ya kugawanya eneo la Bonde la ufa inalenga kuboresha oparsheni za kiusalama katika eneo hilo, baada ya kushuhudia changamoto haswa za vita vya kiukoo zinazosababishwa na masuala ya ardhi.