Wakaazi katika Kaunti ya Mombasa wameshinikizwa kutoa ripoti za washukiwa wa uhalifu kwa maafisa wa polisi ili kuimarisha usalama wa kaunti hiyo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohamed Khalifa alisema kuwa wazazi wanafaa kuwa katika mstari mbele kwa kuwataja wahalifu kwa maafisa wa polisi ili watiwe nguvuni.
Kiongozi huyo wa kidini pia ametoa wito kwa viongozi wote hususan wale wa kidini na jamii kwa ujumla kushirikiana na vitengo vya usalama katika Kaunti ya Mombasa ili kukomesha uovu kabla mji wa Mombasa kutawaliwa na makundi ya kihalifu ya vijana.
"Tunawaomba wazazi pamoja na viongozi wa kidini na wale wa serikali kushirikiana na maafisa wa polisi kwa kuwaripoti washukiwa wa uhalifu ili watiwe nguvuni na kusitisha uhalifu katika Kaunti ya Mombasa,” alisema Sheikh Khalifa.
Kauli ya Kiongozi huyo wa kidini inajiri baada ya maeneo ya Kisauni, Majengo, Mvita na Bamburi kukumbwa na changamoto za kiusalama zinazosababishwa na makundi ya vijana wahalifu.