Chifu mstaafu Justus Ong'era ameunga mkono mpango wa Nyumba Kumi wenye nia ya kudumisha usalama katika maeneo ya makaazi.
Akihutubu kwenye hafla ya mazishi katika eneo la Nyaronge siku ya Alhamisi, Ongera alisema kuwa mpango huo utasaidia wakaazi pakubwa katika kuwatambua washukiwa wa uhalifu na kutoa ripoti kwa maafisa wa polisi.
Ong’era alisema kuwa mpango huo sio mpango mpya kwa kuwa machifu na manaibu wao wamekuwa wakiutekeleza kutoka siku za awali.
"Mimi hushangazwa na baadhi ya watu wanaopinga mipango ya serikali kila mara hata kama ni ya manufaa kwetu. Mpango wa Nyumba Kumi utatusaidia sana kukabiliana na visa vya uhalifu katika jamii,” alisema Ong'era.
Ong'era alisema kuwa mpango huo utasaidia pakubwa kupunguza visa vya uhalifu kwa kuwa wananchi wataiwezesha serikali kuwatambua wahalifu na kisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Alisisitiza kuwa sharti maafisa wa utawala wa zamani wahusishwe kikamifu ili mpango huo kufanikiwa kwa kuwa wana tajriba yakutosha.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukiishtumu serikali kwa kushindwa kuimarisha usalama miongoni mwetu. Kupitia kwa mpango huu wa Nyumba Kumi, tunaweza kuwakabili wahalifu na kisha kuwawasilisha kwa maafisa wa polisi,” alisema Ong'era.
Aliongeza, “Himizo langu kwa serikali ya kitaifa ni kuhakikisha kuwa maafisa wa zamani wa utawala wanahusishwa kikamilifu kwenye mpango huo kwa maana wana tajriba itakayo saidia kuimarisha usalama miongoni mwa wananchi."