Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wenyeji mjini Subukia wamepongeza idara ya polisi kwa kumfuatilia na kumtia mbaroni mwanamme mwenye umri wa miaka 23 katika kituo cha kibiashara cha Kabazi, na kisha kumfikisha mahakamani mara moja kwa kuhusika na mauaji ya babu na nyanya yake Subukia.

Moses Kamau Githuku alikamatwa Jumatano huko Kabazi na kisha Alhamisi akafikishwa mahakamani mbele ya hakimu mkuu Nyakundi Maroro, aliposhtakiwa kwa mauaji ya mkongwe Peter Kaboga Muchu aliyekuwa na miaka 90, na Hannah Njeri Kaboga aliyekuwa na umri wa miaka 85.

Hata hivyo hakukanusha wala kukubali mashtaka dhidi yake, baada ya upande wa mashtaka kuomba azuiliwe zaidi katika kituo cha polisi cha Kirengero, ili kutoa fursa ya uchunguzi zaidi kufanyika.

Ombi hilo lilikubalika ambapo mahakama iliamrisha afikishwe mahakamani Disemba 30, 2015.

Wakizungumza na mwandishi huyu, wakaazi wa Subukia walielezea kuishiwa na hofu iliyokuwa ikitanda kutokana na kutotiwa mbaroni kwa mshukiwa.

“Nilikuwa situmi watoto dukani kwa hofu kwamba huyo kijana anaweza kuwavaamia. Hata mvua ikinyesha kama kulivyonyesha alipowaua wakongwe hao, hofu inanigumbika” Mercy Njeri alisema.

Mauaji hayo yalitekelezwa tarehe 15 disemba,2015