Watu walio na makaazi karibu na Msitu wa Menengai waeonywa dhidi ya kuharibu msitu huo kwa kukata miti na kuwalisha mifugo wao msituni humo.
Naibu afisa msimamizi wa msitu huo Joseph Kiptich, alisema kuwa baadhi ya wakaazi wamekuwa wakishiriki katika shuguli za kuchoma makaa msituni humo, jambo ambalo amesema limepelekea uharibifu wa karibu nusu ekari ya msitu huo.
Akiongea alipowaongoza maafisa wa misitu kukagua uharibu wa msitu huo, Kiptich alisema kuwa uhaba wa maafisa wa kulinda misitu pia umechangia katika uharibifu huo.
“Kuna raia ambao wanakaa karibu na huu msitu na wanafanya biashara ya kuchoma makaa na kulisha mifugo ndani ya msitu huu, hali iliyoleta hasara,” alisema Kiptich.
Aliongeza, “Hatuna maafisa wa kutosha wa kulinda misitu na hii inawapa baadhi ya wakaazi nafasi kubwa kuingia msituni na kufanya uharibifu. Tunapozungumza, unaweza jionea ile hasara wamesababisha kwa kukata miti.”
Kiptich alisema kuwa juhudi za shirika la msitu nchini kupanda miche zaidi msituni humo zimelemazwa na baadhi ya wakaazi wanaong’oa miche hiyo mara tu inapopandwa.
“Kila wakati tunapopanda miche, unapata watu wameachilia mifugo wao kuja kuharibu miche hiyo na hatua hiyo inaturudisha nyuma sana katika juhudi zetu za kulinda msitu huu,” alisema Kiptich.
Aidha, alisema kuwa changamoto nyingine ni mioto inayowashwa na wakulima na wanaolisha mifugo msituni humo haswa nyakati za msimu wa ukame.