Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Mombasa Padri Wilbard Lagho amewashauri waumini wa dini ya katiloki Mombasa kuliombea taifa hili, hasa wakati huu ambapo kanisa linaadhimisha kipindi cha kusali na kufunga kinachofahamika kama Kwaresma.

Kulingana na Padri Lagho, taifa hili limeshuhudia misukosuko mingi hasa ya ukosefu wa usalama, ufisadi, mauaji na dhulma nyingi za kijinsia. Alisema kuwa hatua hiyo itabadili fikra za baadhi ya viongozi na kuwahimiza kuungana pamoja.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Padri Lagho alisema kuwa jukumu la waumini ni kuliombea taifa hili pamoja na kuungana pamoja na viongozi wa tabaka mbalimbali nchini kuleta uiano na utangamano nchini.

“Tumeona kuwa kuna haja ya waumini kushauriwa kuliweka taifa hili katika maombi ili Mungu atuunganishe pamoja na kuleta amani na uiano kwa sababu tumeshuhudia mambo mengi yanayosababisha masikitiko makubwa kwa taifa letu,” alisema Lagho.

Wakati uo huo, Kiongozi huyo wa kidini aliwashinikiza viongozi wa kisiasa kujiweka katika unyenyekevu na kumuomba Mungu kuwaongaza vyema katika kutekeleza masuala muhimu ya kimaendeleo nchini.